Mtu anayesikia luga ya wanyama

O homem que compreende a linguagem dos animais

​Watu huadisia hadisi hii. Mtu moja alienda kumtafuta bibi yake aliyemkimbia. Alipofika kwenye masanganjia akamkuta mbwa mmoja. Huyu akamuuliza: ‘’Unakwenda wapi?”

— Mambo ya kushangaa! Mtu akasema. Sijaona mbwa anayesema.

— Ndio! Uko na haki ya kushangaa, akasema mbwa. Mimi ninajua kama unakwenda kumtafuta bibi yako, na uko wewe peke. Bali haifai kwenda peke yako unapokwenda kumtafuta mke wako.

— Nifanye je, basi? Akasema mtu huyo.

— Nitakwenda nawe, akasema mbwa. Tutakapofika nyumbani kwa wakwe wako, usiseme kama mimi ni mbwa. Na nitakuelezea siri moja: kwa kuwa unasikia maneno yote ninayosema, tangu leo utasikia luga ya wanyama wote; ila, usimuelezee hata mtu moja kama unaweza kuelewa luga ya wanyama. Kama unasema kwamba unaelewa luga ya mbuzi na kuku, utakufa.”

— Sawa tu, kasema mtu huyo. Twende basi.”

— Tutakapofika kule, usiwaache watu kunipa chakula pembeni sababu mimi niko mbwa. Waombe watutandikie meza, tule wote pamoja.

Wakafika mgini wa bibi. Wakakaribishwa na kutayarishiwa chakula. Wakaleta sehemu mbili ya ugali: moja katika kitunga kizuri, na ingine katika chombo kichafu sana. Mtu na mbwa wakala pamoja katika sahani moja. Wakaacha sehemu iliyotiliwa mbwa. Wageni walipokwishakula, watu wakakata majani ya migomba ili kutandika kitanda kwa wageni na akawasukuma mbuzi (wakawaswaka) warudie mgini.

Mbuzi wakatoka porini walikokuwa. Walipofika mgini, wakaanza kunungunika: « Nyumbani humu mna wageni, kwa sababu walikonga moto! » Mbuzi mwingine akasema: « Aa! Ole kwa watoto wetu! » Mabeberu walinungunika vilevile, wakisema: « Oo! Msinungunike: Kati yetu ndio watachagua wale watakaokufa! » Mbuzi jike wakasema: « Msinungunike nyinyi, kwa sababu hamna watoto; sisi wenyi watoto, tutaona tabu! ». Mabeberu wakajibu: « Nyinyi mbuzi jike, munaweza kuwa na bahati, kwa sababu wanaweza kuwaacheni wazima na kuchinja watoto wenu! »

Mtu akaanza kucheka kwa kusikia hayo yote, na hakuweza kunyamaza. Kuku nao wakarudia nyumbani. Wakalalamika na kusema: « Ole wetu! Ole kwa watoto wetu! Kumefika wageni tena! » Moja wao akamwambia mwenziwe: « Usilie! hauwezi kuogopa kitu; uko unaatamia; hawatakuchinja. »

Ndipo Mbwa akamwambia mtu: « Sikukuambia kama utasikia luga ya wanyama? »

Wakalala; usiku ukakucha. Mtu akamwambia mke wake: « Bibi yangu, njoo tuondoke. » Mke naye: « Ngoja niende kukatia mama kuni. » Mama huyo alikuwa chongo. Mtoto wake akamuomba alinde kalanga alizoanika anika. Mama akatoka nyumbani, akaja kukaa kwenye kalanga ili kuzilinda. Mkwe wake pia aliketi nje na mbwa wake. Kuku wakafika, wakaitana wakisema: « Njooni, rafiki, njooni tukale kalanga. Mwenyi kulinda kalanga ni chongo. »

Mtu hakuweza kunyamaza: akapasuka na cheko. Nao kuku waliongeza kusema: « Kuleni kalanga zenyi kuwa upande wa jicho mbovu. Akigeuza kichwa, itafaa kukimbia! » Ndipo mtu akaanguka kifudifudi chini ya kiti, kwa kicheko.

« Aa! Mkwe wangu ananichekelea, kwa sababu niko chongo », akasema mama mkwe. Huyu akakasirika na akaingia nyumbani. Na kuku walipoona hivyo, wakala kalanga zote. Mke wa mtu alipotoka huko mwituni, alishangaa: « Mama, mbona uliingiza kalanga na jua haijalala? »Naye mama akasema: « Mume wako alichekelea chongo yangu; nikaingia nyumbani na kalanga zote zikaliwa. Hapo ndipo zilikuwa kalanga. »

— Ndiyo kusema kalanga zote zimepotea! Shamba nzima!

— Ndio!

Mwanamke akamkasirikia mume wake kwa kuwa alimchekelea mama yake: « Kwa sababu gani ulimchekelea mama na japo ulikuja kunitafuta? Ni kweli unanipenda wewe unayemchekelea mama aliyenizaa? » Bwana akaapa na kuapiza ya kuwa hakumchekelea mama yake. Lakini bibi akaongeza kusema: « Wakati ulikuwa unaanguka kifudifudi, ulikuwa na mtu mwingine gani? Niambie basi ulimchekelea nani! ». « Ole wangu! », akasema bwana. Mwanamke alikasirika mno hata kutaka kujiua. Ndipo bwana akamuelezea haya: « Nilicheka kwa sababu hii: kuku walikuwa wakisema: « Tule kalanga zenyi kuwa upande wa jicho bovu. Ndiyo sababu nilicheka. » Na akawafasiria yote aliyonena mbwa njiani. Na alipomaliza kusema akazimia. Naye mbwa akarejea kwake.

Ndio sababu haifai kamwe kumchekelea mtu anaposema.